Dar es Salaam. Watafiti nchini wametakiwa kuhakikisha kazi zao zinajikita katika kutoa majawabu ya kisayansi dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi na athari zake, upotevu wa bio-anuai, uhifadhi wa rasilimali na mazingira na nyinginezo.
Majawabu hayo ya kisayansi yanayotokana na tafiti yametajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Hayo yameelezwa leo Aprili 1,2025 na wadau walioshiriki katika mkutano wa kuadhimisha miaka 50 ya jarida la Sayansi la Tanzania Journal of Science (TJS) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mkutano huo wa siku mbili, ambao umekusanya takriban wadau 200 kutoka ndani na nje ya nchi, unalenga kutathmini safari ya miaka 50 ya utafiti tangu kuanzishwa kwa jarida hilo mwaka 1975.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema watafiti nchini wana jukumu la kuhakikisha kuwa tafiti wanazozifanya zinakuwa chachu ya kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, amesisitiza kuwa dira hiyo inategemea kwa kiasi kikubwa matumizi sahihi ya sayansi, tafiti teknolojia na ubunifu.
Mushi amebainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, Tanzania inalenga kukuza uchumi wake kutoka kiwango cha sasa na kufikia uchumi wa dola za Marekani trilioni moja.
Ameeleza kuwa malengo hayo yanaenda sambamba na azma ya kuongeza kipato cha kila mtu kwa mwaka kufikia wastani wa dola 7,000.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo, mafanikio hayo hayawezi kufikiwa bila kuongeza tija katika nyanja zote za uzalishaji kupitia tafiti zenye tija, ambapo jarida la TJS linapaswa kuwa jukwaa muhimu la kuwezesha nchi kutumia vizuri sayansi na ubunifu.
Katika hatua nyingine, Profesa Mushi alitumia fursa hiyo kutoa tahadhari kwa watafiti na wahariri wa majarida ya kitaaluma kuhusu changamoto zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia, hususan matumizi ya Akili Unde.
Amehimiza washiriki wa mkutano huo kuwa na uelewa mpana wa matumizi sahihi ya teknolojia hiyo ili kukabiliana na hatari ya kuchapisha taarifa ambazo hazikutokana na utafiti halisi.
“Watafiti wasiokuwa makini wanaweza kutumia Akili Unde kutengeneza taarifa za uongo, jambo ambalo linaweza kuharibu sifa na uaminifu wa majarida ya kisayansi nchini,” amesema.
Naye Mratibu wa mkutano huo, Profesa Andrew Macrice kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa lengo si kusherehekea tu mafanikio yaliyopatikana, bali ni kuweka mikakati thabiti kwa miaka 50 ijayo,.
Amesisitiza kuwa watafiti wamejipanga kutoa masuluhisho ya changamoto zinazoikabili jamii kwa sasa, ikiwemo upotevu wa ardhi, mabadiliko ya tabia nchi, uhaba wa chakula, na upotevu wa bio-anuai.
Profesa Macris ameongeza kuwa tafiti zinazochapishwa sasa zinapaswa kuleta maendeleo endelevu ili kuhakikisha vizazi vya sasa na vijavyo vinanufaika na rasilimali za Taifa.
“Nafasi ya watafiti katika dira ya 2050 ni kuhakikisha kila utafiti unaofanywa unajibu kero za wananchi na kuendana na vipaumbele vilivyoainishwa katika dira hiyo ya Taifa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amebainisha kuwa sayansi haipaswi kuishi peke yake, bali ni lazima ishirikiane na jamii na kusaidia katika utungaji wa sera zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja.
Profesa Anangisye ameeleza kuwa jarida la TJS limekuwa nyenzo muhimu katika kuwajenga wanasayansi chipukia na kutoa jukwaa la kubadilishana mawazo ya kitaaluma.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa watafiti vijana kutumia maadhimisho haya kama chanzo cha msukumo katika kukuza taaluma zao.
Jarida la TJS, ni miongoni mwa majarida 27 yanayomilikiwa na UDSM, limetajwa kuwa na mafanikio kwa kuweza kuingia katika mfumo wa kimataifa wa machapisho.
