Wafanyabiashara Kariakoo wamgomea Chalamila, wafunga maduka

LICHA ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuwataka wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kuepuka kushiriki mgomo uliovuma kuanza leo, hali katika soko hilo imeonesha wafanyabiashara hao wamegomea agizo hilo na kufunga maduka. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo imekuja siku mbili baada ya kusambaa kwa vipeperushi katika mitandao ya kijamii vikielekeza wafanyabiashara wote wa soko hilo kufunga biashara zao na maduka yao bila kikomo kuanzia leo Jumatatu hadi pale serikali itakapotatua kile walichodai changamoto zaoza kibiashara.

Timu ya MwanaHALISI iliyopiga kambi katika viunga mbalimbali vya soko hilo, imeshuhudia maduka hayo yakiwa yamefungwa hadi saa nne asubuhi kila kona hapakuwa na biashara yoyote.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kuhaha kutafuta huduma huku polisi wachache wakipiga doria katika viunga vya soko hilo.

Hali ilivyo katika baadhi ya maduka Kariakoo

Juzi Jumamosi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Khamisi Livembe alikanusha kuwepo kwa mgomo huo wa wafanyabiashara na kusisitiza taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao kuhusu mgomo huo hawaitambui na amewasiliana na wafanyabiashara wote nao hawatambui aliyetoa taarifa hiyo.

Naye Chalamila akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili aliwataka wafanyabiashara kutambua kuwa mgomo sio suluhisho pekee la kutatua changamoto bali utaratibu bora wa kutatua changamoto ni kukaa mezani na mamlaka kujadili kwani mgomo huongeza chuki na wakati mwingine kusababisha uvunjifu wa amani.

RC Chalamila

Chalamila alisema kuwa Serikali inatambua changamoto za wafanyabiashara na kada zingine za wafanyakazi na watumishi na inaendelea kuzifanyia kazi.

Aliwataka wafanyabiashara kushirikiana na Serikali kumaliza changamoto zao na kuepuka mihemko inayoanzishwa na watu wachache wasio kuwa na nia njema na Mkoa wa Dar es salaam na Taifa kwa ujumla.