Iran Yatangaza Kulenga Kampuni za Teknolojia za Marekani Mashariki ya Kati

Global Publishers
April 1, 2026
0 Comments

Wakati mvutano wa vita ukiendelea, Iran kupitia Jeshi lake la Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) limetangaza mpango wa kulenga makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani yanayofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.

Katika taarifa iliyochapishwa na chombo chake rasmi cha habari, Sepah News, IRGC imetaja jumla ya kampuni 18 ambazo inadai zinahusika kwa namna moja au nyingine katika kupanga na kufuatilia malengo ya mashambulizi ya Marekani. Miongoni mwa makampuni yaliyotajwa ni Apple, Microsoft, Google pamoja na mengine makubwa kama Meta, Nvidia, Oracle, Tesla, HP, Intel na IBM.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, IRGC imewataka wafanyakazi wa makampuni hayo kuondoka mara moja katika maeneo yao ya kazi, ikibainisha kuwa mashambulizi dhidi ya kampuni hizo yatarajiwa kuanza siku ya Jumatano saa 8:00 usiku kwa saa za eneo husika.

Iran imesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati yake katika kujibu mashinikizo yanayoendelea katika vita vinavyoendelea, huku ikizitaja kampuni hizo kuwa na mchango katika shughuli zinazohusiana na usalama na operesheni za kijeshi za Marekani.

Hata hivyo, hatua hii imezua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa miundombinu ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya akili mnemba (AI) katika kanda hiyo, hasa kutokana na ukweli kwamba mataifa kama Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia yamekuwa yakivutia uwekezaji mkubwa wa kiteknolojia katika miaka ya hivi karibuni.