Mwanza. Licha ya kuendelea kulalamikiwa kwa mikopo yenye masharti magumu, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza bado hawaoni riba kubwa kama tatizo, hali inayochangia kuendelea kuathirika kifedha kutokana na ukosefu wa uelewa sahihi wa masuala ya mikopo.
Kutokana na hali hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua kampeni ya ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’ yenye lengo la kutoa elimu ya fedha kwa umma ili kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kabla ya kukopa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Aprili Mosi, 2026 Kaimu Mkurugenzi wa Tawi na Meneja wa Uchumi BoT Mwanza, Isa Pagali amesema mikopo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo iwapo itatumika kwa uelewa sahihi, lakini bila elimu ya kutosha inaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya kifedha.
Amesema changamoto kubwa iliyopo ni kuwa wananchi wengi wamezoea mazingira ya mikopo isiyo rasmi kiasi cha kuona baadhi ya masharti yasiyo sahihi kuwa ni ya kawaida.
Kaimu Mkurugenzi wa Tawi na Meneja wa Uchumi BOT Mwanza, Isa Pagali akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’ yenye lengo la kutoa elimu ya fedha kwa umma ili kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kabla ya kukopa. Picha na Saada Amir
“Watu wanaweza kuwa na maumivu ndani lakini wasijitokeze, mara kadhaa tunakutana na wanaolalamika wanajikuta hawawezi kumudu uwezo wa kulipa madeni makubwa ambayo yanakuwa kwa muda mfupi kutokana na taratibu zisizo sawa.
“Wengi waliotufikia hawaoneshi kwamba kupanda kwa gharama kwa haraka ni kama tatizo…gharama kama riba, faini mbalimbali wanazozitoza watoa huduma kutokana na kushindwa kulipa riba kubwa, kwa hiyo riba kubwa siyo tatizo wengi wameonesha hivyo lakini kwetu sisi tunaona ni tatizo,”amesema Pagali.
Amewataka wahitaji wa mikopo wasikubali kukopa kwa mkopeshaji asiye na leseni ya BoT, bila kuelewa masharti, kutosoma kila kitu kabla ya kusaini, kutambua masharti ya mkopo, uwezo wa kurejesha na madhara ya kuchelewa au kushindwa kulipa.
“Na hakikisha unakopa kwa lengo la maendeleo sio kwa presha au ushawishi…walaji wa huduma hizi za kifedha wanahimizwa kujitokeza kwa wingi wapate elimu hii ili waweze kujiepusha kuingia kwenye mikopo umiza,”ameeleza.
Meneja Msaidizi wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka BOT Dar es Salaam, Mary Ngassa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’ itakayofanyika kwa siku 20 mkoani Mwanza. Picha na Saada Amir.
Meneja Msaidizi wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha wa BOT Dar es Salaam, Mary Ngassa amesema kampeni hiyo ya siku 20 itafanyika mitaa yote ya Mkoa awa Mwanza, ikiwemo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na maeneo yanayoshukiwa kuwa na watoa mikopo wasiosajiliwa.
“Kampeni hii inalenga kuondoa mikopo umiza na kausha damu, mtu anakaushwa damu ama anaumizwa kwa kuwa hana uelewa, hajui wajibu wake na hajui nini cha kufanya anakuwa anaonewa…kampeni hii inaenda kumwelimisha na kupanua uelewa wake kwenye masuala ya mikopo,” amesema Ngassa.
Aidha, BOT imeonya kuwa watoa huduma za kifedha wanaofanya kazi bila leseni wanakiuka sheria na wanaweza kuchukuliwa hatua kali, ikiwemo kutozwa faini ya kati ya Sh20 milioni hadi Sh100 milioni au kifungo cha miaka mitatu hadi mitano jela, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Kifedha ya mwaka 2018.
Mkazi wa jijini Mwanza, Charles Marwa amesema alikopa Sh1 milioni lakini alijikuta analipa karibu mara mbili ya kiasi hicho kutokana na masharti ya mkopo.
Ameongeza kuwa watoa mikopo wengi hutumia hali ya uhitaji wa haraka wa fedha kwa wananchi kuwashawishi kusaini mikataba bila maelezo ya kina, hali inayowaacha wakopaji katika mzigo mkubwa wa madeni.
