Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kulihutubia taifa leo usiku akiwa na kile Ikulu ya White House imeeleza kuwa ni taarifa muhimu kuhusu vita vinavyoendelea nchini Iran.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, hotuba hiyo itatolewa majira ya saa 9:00 usiku kwa saa za Marekani (ET), ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu mada atakayozungumzia Rais Trump.
Hatua hiyo inakuja baada ya Trump kunukuliwa na vyombo vya habari akisema katika mahojiano kwamba Marekani inaendelea vizuri katika mzozo huo na kwamba vita vinakaribia kufikia tamati. Pia alidokeza kuwa Marekani inaweza kujiondoa katika eneo hilo ndani ya wiki mbili hadi tatu zijazo, akisisitiza kuwa Iran haina lazima ya kufanya makubaliano na Marekani ili mapigano yaishe.
Hata hivyo, kauli hizo zimekuja katika kipindi ambacho hali ya sintofahamu inaendelea, kufuatia madai kwamba Marekani na Iran zilikuwa katika mazungumzo ya awali, huku Iran ikikanusha kuwepo kwa mazungumzo yoyote ya moja kwa moja na Washington.
Vita hivyo vimeingia mwezi wake wa pili, na tayari vimesababisha vifo vya wanajeshi wa Marekani wapatao 13, huku karibu 350 wakiripotiwa kujeruhiwa tangu mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yalipoanza Februari 28, kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani aliye na taarifa za operesheni hizo.
Wakati huohuo, athari za vita hivyo zimeanza kuhisiwa na wananchi wa Marekani, ambapo bei ya mafuta imeendelea kupanda na kufikia zaidi ya dola 4 kwa galoni, kiwango cha juu zaidi tangu mwaka 2022. Hali hiyo inachangiwa na usumbufu katika eneo la Strait of Hormuz, ambalo ni njia muhimu inayopitisha takriban robo ya mafuta yanayotumika duniani.
Uchumi na hali ya maisha ya wananchi wa Marekani pia imeendelea kuwa mjadala mkubwa, huku baadhi ya wananchi wakielezea kutoridhishwa na namna serikali inavyolishughulikia suala hilo, hasa kutokana na ongezeko la gharama za nishati.
Hotuba ya leo ya Trump inatarajiwa kutoa mwanga kuhusu mwelekeo wa Marekani katika vita hivyo, pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika siku zijazo.