JITIHADA ZA RAIS SAMIA ZA ZIDI KUINUA SEKTA YA UTALII

………

Na Sixmund J. Begashe, Dodoma

Jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zimetambuliwa kitaifa, kikanda na kimataifa zimechechemua kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa watalii nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Bungeni Jijini Dodoma kwenye hotuba yake kuhusu Mapato na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2026/2027.

Dkt. Mwigulu amesema kutokana na uhuhimu wa Sekta ya Maliasili na Utalii katika ukuaji wa uchumi, ajira na pato la Taifa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuinua sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.

“Mikakati hiyo imeongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa kwa asilimia 10.73 kutoka watalii 5,360,247 mwaka 2024 hadi 5,935,561 mwaka 2025 na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024 hadi dola za Marekani bilioni 4.4 Desemba 2025 sawa na ongezeko la asimilia 12.82”. Dkt. Mwigulu

Katika kikao hicho cha 3 cha Bunge la 13 kilichoudhuriwa pia na Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Mhe. Dkt Mwigulu ameongeza kuwa katika kutambua mchango mkubwa wa Mhe. Rais Samia katika sekta ya Maliasili na Utalii, tarehe 31 Januari, 2026, Mheshimiwa Rais alitunukiwa tuzo ya Kiongozi Mwenye Maono katika hafla ya utoaji tuzo ya Serengeti Awards.