Kigogo Baraza la Usalama wa Taifa afariki dunia

Dar es Salaam. Mratibu Msaidizi Baraza la Usalama wa Taifa, Brigedia Jenerali Vitalis Chakila amefariki dunia Jumapili Juni 23, 2024 akiwa na miaka 59.

Taarifa za kifo cha Chakila zimetolewa leo Jumanne Juni 25, 2024 kupitia taarifa kwa umma iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Ilonda.

Taarifa hiyo inasema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda anasikitika kutangaza kifo cha Brigedia Jenerali Vitalis Andrew Chakila.

Brigedia Jenerali Chakila atazikwa Alhamisi Juni 27, 2024 Kahama mkoani Shinyanga.

“Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa Makao Makuu ya Jeshi, Msalato jijini Dodoma tarehe Juni 26, 2024 saa tano (5:00) asubuhi, na baadaye kusafirishwa kuelekea Kahama mkoani Shinyanga kwa mazishi yatakayofanyika Juni 27, 2024,”imesema taarifa hiyo.

Wasifu wa Brigedia Jenerali Chakila jeshini

Katika miaka yake 36 ya utumishi jeshini, Brigedia Jenerali Chakila amehufumu katika nafasi mbalimbali tangu ajiunge na JWTZ mwaka 1987.

“Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tarehe Septemba 30, 1987. Alihudhuria kozi ya Ofisa Mwanafunzi nchini Tanzania na kutunukiwa kamisheni mwaka 1989. Alipata mafunzo mengine ya kijeshi nchini Uholanzi, Mali na Tanzania kwa nyakati mbalimbali,”inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika kipindi cha utumishi wake jeshini, alipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali hadi cheo cha Brigedia Jenerali alichopandishwa Aprili 12, 2018.

“Aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwamo ya Mkuu wa Tawi la Ukaguzi Makao Makuu ya Jeshi mwaka 2020 hadi 2021 na Mratibu Msaidizi Baraza la Usalama wa Taifa mwaka 2021, madaraka aliyohudumu hadi alipofariki dunia tarehe Juni 23, 2024,”inaeleza taarifa hiyo.

Katika utumishi wake jeshini, Brigedia Jenerali Chakila ametunukiwa medali mbalimbali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.

“Alimtunukiwa medali mbalimbali pamoja na miaka 40 ya JWTZ, Comoro, utumishi mrefu Tanzania, utumishi uliotukuka Tanzania, miaka 50 ya Uhuru, miaka 50 ya Muungano, miaka 50 ya JWTZ, miaka 60 ya Uhuru na miaka 60 ya Muungano,”inaeleza taarifa hiyo ya JWTZ.

Brigedia Jenerali Chakila alizaliwa Mei 29, 1965 katika Kijiji cha Mhungula, Kata ya Nyihogo, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Wavulana Bwiru na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1984.

Aliendelea na elimu ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Kibaha iliyopo mkoani Pwani na kumaliza mwaka 1987 kisha kujiunga na jeshi.