NEMC: Lipeni ada ya tathmini ya mazingira kwa wakati

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka watathmini mazingira na wawekezaji kulipa Ada za Tathmini ya  Mazingira (EIA) katika wakati uliopangwa ili kutekeleza miradi yao kwa kuzingatia sheria za mazingira.

NEMC imesema muda unaotakiwa kulipwa ada na tozo hiyo kisheria ni kuanzia Julai mosi hadi Desemba 31 kila mwaka, hivyo kutozingatria muda kutakwamisha miradi husika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 25, 2024, wakati anatoa tangazo hilo, msimamizi wa ada na tozo wa NEMC, Canisius Karamaga amesema umuhimu wa tathmini hizo ni kulinda mazingira na viumbe hai akiwamo binadamu.

“Utaratibu wa ada na tozo hii inalipwa mara moja kwa mwaka kuanzia Julai mosi hadi Desemba 31 ili kuiwezesha NEMC kupokea fedha hizo katika kipindi hicho cha miezi sita na iweze kusimamia na kuishauri jamii namna ya kuhifadhi mazingira kwa wakati.

“Unaweza kulipa katikati Agosti, Oktoba lakini mwisho lazima iwe Desemba 31 na baada ya hapo ikitokea mtu hajalipa baada ya muda huo kuanzia Januari hadi Juni ya mwaka wa fedha itaambatana na adhabu ya asilimia tano ya fedha,” amesema Karamaga. 

Amesema ili kutekeleza majukumu hayo imeundwa kanuni ya ada na tozo ya mwaka 2021 inayoelezea wajibu wa watu kulipa na anayetakiwa kulipa

“Lengo la ada na tozo ni kupata fedha kwa waendelezaji wa miradi na wafanyaji wa shughuli mbalimbali ili ziweze kukaguliwa na kupata miongozo inayokubalika ikiwaemo tathimini ya athari za mazingira.”

Kamaraga amesema wanapofanya tathimini hiyo inasaidia kuona ni madhara gani yanaweza kujitokeza iwapo utafanya uendelezaji huo na mhusika anapaswa kufanya mambo gani ili kuepuka athari hizo.

Meneja Mawasiliano kwa Umma kutoka NEMC, Irene John amesema taasisi hiyo kwa kuwa imepewa jukumu hilo la usimamizi na uhifadhi wa mazingira shabaha yake ni kuona mazingira yanaendelea kuwa rafiki.