Vituo vya msaada kisheria vilivyosaidia jamii kupata haki

Unguja. Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim amewataka wanajamii kuvitumia vituo vya msaada wa kisheria katika maeneo yao kupunguza gharama na kufuata huduma masafa marefu.

Akifungua kongamano la vyuo vikuu kuhusu msaada wa kisheria lililofanyika Tunguu, Zanzibar leo Juni 26, 2024, Jaji Ibrahim amesema lengo la Serikali kuanzisha vituo hivyo ni kuondoa usumbufu uliokuwepo, akiitaka jamii kuvitumia.

“Kabla ya kuwepo wasaidizi wa sheria katika jamii watu wengi walikosa msaada kisheria, jambo lililosababisha kukosa haki zao, kwa hiyo ni vyema kuvitumia vituo hivi viwasaidie,” amesema Jaji Ibrahim.

Amesema watu wengi hawana uwezo wa kuwalipa mawakili lakini kupitia msaada wa kisheria wanajengewa ujasiri wa kupambania haki zao.

Ameipongeza idara ya katiba na msaada wa kisheria kuandaa kongamano hilo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, akieleza litasaidia kuhamasisha upatikanaji wa huduma katika ngazi ya jamii na vyuo vikuu.

Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said amesema madhumuni ya kongamano hilo ni kuwajengea uzalendo, kujitolea na kuisaidia jamii kupitia msaada wa kisheria.

Amewataka wanafunzi kuwaunga mkono katika shughuli zilizoandaliwa na idara hiyo katika wiki ya msaada wa kisheria hadi kufikia kilele Juni 28.

Amewashukuru wadau wa maendeleo wakiwamo UNDP na LSF kwa kuwaunga mkono na kuhakikisha jamii inapata haki kupitia msaada wa kisheria.

Awali, akitoa salamu za Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mratibu na mshauri wa programu za utawala bora, Godfrey Mulisa amesema shirika hilo litaendelea kuisaidia Serikali kupitia idara hiyo, kutoa elimu ya msaada wa kisheria ili wananchi wapate stahiki zao.

“Haki ya kupata msaada wa kisheria ni ya kila mtu, hivyo niwaombe muwafikie watoa huduma za msaada wa kisheria waliopo katika maeneo yenu,” amesema.

Kaimu Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Zanzibar, Dk Sikujua Omar Hamdan amesema kuwapo vituo vya msaada wa kisheria vyuoni kunasaidia kujenga weledi na uzoefu kwa wanafunzi wa kada ya sheria kuisoma kwa vitendo fani hiyo.

Mmoja wa wanafunzi wa sheria Chuo cha Taifa Zanzibar (Suza), Zulkhat Haji amesema hatua hiyo ni moja ya mafunzo kwa vitendo, hivyo kuwataka wanafunzi wenzake kuitumia fursa hiyo kujifunza kwa bidii. 

Mada tatu zilijadiliwa katika kongamano hilo, ambazo ni dhana ya msaada wa kisheria, athari za dawa za kulevya kwa vijana na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na namna ya kuwalinda waathirika.

Kongamano hilo limewashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu.