KUNDI la mawakili na wanaharakati wameelekea mahakamani kumzuia Rais wa Kenya, William Ruto kutia saini Muswada wa Fedha wa 2024 na Muswada wa Kibali cha Matumizi ya Fedha wa 2024. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Mawakili saba wakiwemo Ndegwa Njiru, Jackline Mwangi, Lempaa Suyinka na Chama cha Wanasheria wa Mlima Kenya wanataka mahakama itoe maagizo ya kumzuia Rais Ruto kutia saini miswada hiyo hadi kesi yao itakaposikizwa na kuamuliwa.
Muswada huo wa fedha ulipitishwa na Bunge la Kitaifa jana Jumanne licha ya maandamano ya kuupinga yaliyoshuhudiwa jijini Nairobi na kaunti zingine 36.
Kwa mujibu wa sheria, Rais Ruto anapaswa kutia saini Miswada hiyo kuwa sheria ndani ya siku 14 baaada ya kupitishwa na bunge.
Hata hivyo, anaweza kuikataa na kuirejesha bungeni pamoja na taarifa inayotaja sehemu ambazo angetaka zifanyiwe mabadiliko.
Ikiwa Ruto atasaini kushughulikia miswada hiyo miwili itakuwa sheria siku 14 baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa kuiwasilisha kwake.
Mwaka wa kifedha wa 2024/2025 unaanza tarehe 1 Julai na inatarajiwa kwamba serikali itakuwa ikikusanya ushuru chini ya mwongozo uliotolewa na Muswada wa Fedha wa 2024.
Katika kesi yao, mawakili hao wanadai kuwa mpango wa utayarishaji wa bajeti ulisheheni mabishano baada ya Waziri wa Fedha, Njuguna Ndung’u kuwasilisha Bungeni Muswada wa Fedha wa 2024 tarehe 9 Mei, 2024.
“Kwamba kwa mujibu wa Kipengele cha 222 (1) cha Katiba agizo litolewe la kumzuia Rais William Ruto kutia saini Muswada wa Fedha wa 2024 na Muswada wa Matumizi ya Fedha za Bajeti ya 2024 kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii,” wakasema.
Kupitia wakili Kibe Mungai, watu hao wanasema kuwa maoni ya umma hayakuzingatiwa hususani katika Muswada wa Fedha wa 2024 hivyo inavyohitajika kuendana na kipengele cha 221 (2) cha Katiba.