NYOTA wapya wa Azam FC, Yoro Mamadou Diaby kutoka Yeleen Olympique ya Mali, Adam Adam (Mashujaa) na Wacolombia Jhonier Blanco (Aguilas) na Ever Meza kutoka Leonnes wameanza kupigishwa tizi mapema ikiwa ni siku chache tu kabla ya kuripoti kambini Chamazi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Ever Meza
Wachezaji hao ambao tayari wamejumuishwa katika kundi la Whatsapp la wachezaji wa timu hiyo, wameanza kupewa programu mbalimbali za mazoezi wakati wakimalizia mapumziko kabla ya kila mmoja kuanza kuripoti kambini kuanzia Julai mosi hadi tano.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kwamba programu hizo zimelenga kuwaweka sawa ambao walijisahau katika kipindi ambacho wamepewa mapumziko, ili kila mmoja arejee Chamazi akiwa katika hali nzuri ya utimamu wa mwili kabla ya kuanza mazoezi ya nguvu ya pamoja kama timu.

Adam Adam
Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo anasubiri kwa hamu kukutana na wachezaji hao wapya katika maandalizi ya msimu ujao ambayo anaamini kuwa yatakuwa na nafasi kubwa katika mpango wa timu hiyo kufanya vizuri zaidi msimu ujao.
“Tulihitaji maingizo mapya kwa ajili ya kuongeza nguvu. Naamini tutakuwa na wakati mzuri wa kufahamiana nao vizuri wakati wa maandalizi,” amesema.
Akizungumzia maandalizi yatakavyokuwa, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabit Zacharia maarufu Zaka Zakazi amesema yatakuwa Morocco kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA na safari hii Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo wataicheza kwa mara ya kwanza baada ya misimu 10.
Mara ya mwisho kwa Azam FC kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni msimu wa 2013/14 ilipotwaa ubingwa wa Bara.
“Tutafanya mazoezi Chamazi hadi tarehe saba tutakwenda Zanzibar. Tukifika tutafanya mazoezi siku hiyohiyo hadi Julai 13 tutarudi Dar na tarehe 14 tutaondoka nchini kwenda Morocco kuweka kambi ndefu na hiyo ndiyo ‘pre season’ yetu kwa msimu huu,” amesema Zaka.
Amesema watakaa nchini Morocco hadi mwishoni mwa mwezi Julai ndipo watakaporejea tayari kwa ajili ya kufungua msimu mpya wa mashindano.